YANGA ndani ya dakika 450 za Ligi Kuu Bara imekuwa kwenye kasi yake ya ubora baada ya kuweza kushinda mechi zake zote ilizocheza bila kupoteza.
Ikiwa inanolewa na Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi ilifungua ukurasa wa mechi za ligi kwa kushinda bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar.
Mchezo huo ulichezwa Uwanja wa Kaitaba kisha wakarudi Dar na kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Geita Gold ukiwa ni mchezo wa pili uliochezwa Uwanja wa Mkapa.
Mchezo wa tatu walicheza ugenini ilikuwa dhidi ya KMC na ubao wa Uwanja wa Majimaji, Songea ulisoma KMC 0-2 Yanga.
Walirudi Dar na kucheza mchezo wa nne ilikuwa mbele ya Azam FC na ubao wa Uwanja wa Mkapa ulisoma Yanga 2-0 Azam FC ikiwa ni mwendelezo wa kusepa na pointi tatu kwenye mechi ambazo wamecheza.
Dakika 450 zilikamilishwa Uwanja wa Mkapa uliposoma Yanga 3-1 Ruvu Shooting mchezo ulioshuhudia timu hiyo ikivunja rekodi ya ushindi mkubwa kwa msimu wa 2021/22 ndani ya dakika 90 na nyota wao Diarra Djigui aliruhusu bao kwa mara ya kwanza baada ya kutua ndani ya kikosi hicho cha Yanga.
Kipa huyo raia wa mali aliweza kuweka rekodi ya kucheza mechi nne bila kufungwa jambo ambalo lilikuwa linabebwa na ukuta imara unaoundwa na mzawa Dickosn Job, Bakari Mwamnyeto na Yannic Bangala kutoka DR Congo.
Mtambo wa mabao ni Feisal Salum yeye ametupia mabao matatu na pasi moja ya bao kwa msimu wa 2021/22 na kuhusika kwenye mabao manne kati ya tisa huku Fiston Mayele na Jesus Moloko wakiwa wametupia mabao mawilimawili na Shaban Djuma na Tonombe Mukoko hawa ni wazee wa mojamoja.
Pia Fei Toto ni mfungaji wa kwanza kwa msimu wa 2021/22 ndani ya Yanga bao lake alifunga mbele ya Kagera Sugar kwenye mchezo wa kwanza.

No comments:
Post a Comment