KWENYE upande wa ukuta taratibu Tanzania inazidi kuwa imara ambapo kwenye timu ya taifa uhakika uwepo wa Bakari Mwamnyeto,Shomari Kapombe na Mohamed Hussein huku ngoma nzito ikiwa upande wa washambuliaji.
Wakati tatizo la ushambuliaji likitafutiwa tiba,kuna kijana
mwingine wa kazi katika eneo la ulinzi anaitwa Dotto Shaban yupo zake ndani ya
kikosi cha Tanzania Prisons.
Nyota huyo ameweka wazi
kwamba lengo namba moja ni kuona timu hiyo inabaki kwenye ligi licha ya kuwa
kwenye mwendo usiopendeza huyu hapa:-
“Kweli hatukuanza vizuri kwenye mechi za mwanzo hasa
ukizingatia kwamba kila timu inajipanga kupata pointi tatu na yote ni matokeo
ambayo tulikuwa tunapata.
“Pia hata aina ya mechi ambazo tulikuwa tunacheza zote zilikuwa
ni ngumu hivyo kukosa matokeo kulitufanya tuwe kwenye mwendo ambao
hatukuupenda.
“Hilo liliweza kuonwa na benchi la ufundi liliweza kufanyia kazi
na kuna mechi tulikuwa tunapata matokeo nab ado tunapambana.
Kwa nafasi ambayo mpo kuna nafasi ya kubaki kwenye ligi?
“Nafasi bado ipo unajua ukiziangalia timu ambazo tunacheza nazo
kisha na namna msimamo ulivyo tofauti yake sio kubwa na kila mmoja anaifikia.
“Ambacho tumekubaliana kwa sasa kwa mechi ambazo zimebaki kuweza
kutulia na kufanya vizuri kwa kupata matokeo hilo linatufanya tuweze kubaki
kwenye ligi na hilo ni moja ya lengo letu kubwa.
Ushindani wa msimu huu na uliopita tofauti ipoje?
“Naona msimu huu ushindani umekuwa ni mkubwa tofauti na msimu
uliopita kwani uwekezaji umekuwa mkubwa na timu zilifanya usajili mzuri.
“Kila mechi ambayo sisi tunacheza ni fainali kwani hakuna timu
ambayo tulikuwa tunacheza nayo mchezo unakuwa wa kawaida.
Malengo yako yapoje?
“Kwangu mimi siwezi kujitanguliza ila ninaanza na timu kwanza
kikubwa ni kubaki kwenye ligi hilo ni jambo la kwanza na tunashirikiana kuweza
kulitimiza.
“Baada ya hilo sasa mimi binafsi ni kuweza kufanya kazi kwa
juhudi bila kuchoka katika kutimiza majukumu yetu na hilo lipo kila siku.
“Ninapenda kuweza kucheza siku moja kwenye timu ya Taifa ya
Tanzania ya wakubwa na hiyo ni muhimu kwa ajili ya kulitumikia taifa letu,jambo
hilo lipo na Imani yangu siku moja itawezekana.
Ikiwa mmepoteza ama kushinda muda wa mapumziko mnaambiwa nini?
“Hapo inategemea na mchezo na mbinu ambazo tumeingia nazo katika
mechi, kwa mfano tukishinda tunakwenda na mbinu ya kujilinda zaidi na
kushambulia.
“Tukipoteza mwalimu amekuwa akituambia kwamba makosa ambayo
tumefanya ni kwa sababu ipi,hilo limekuwa likitokea na tumekuwa tukifanya kazi
kwa kusikiliza benchi la ufundi.
Umecheza na Yanga na Simba,tofauti yao ipo wapi?
“Kucheza na hizi timu kubwa kwanza zote zina presha na hakuna
tofauti ila zikiwa Uwanja wa Mkapa hapo kunakuwa na mashabiki wao wengi ambao
wanashangilia mwanzo mwisho.
“Katika upande wa uchezaji kila timu inakuwa na mbinu zake
lakini wagumu kukabika kwa sababu kila unapomaliza kazi ya kumkaba mchezaji
huyu anakuja mwingine katika eneo hilo.
Ratiba yako kwa siku ipoje?
“Ratiba kubwa ni ile ambayo inafanywa na timu kwa kuwa siishi
nyumbani bali ninaishi kambini,huku ni sehemu ambayo tunakuwa na ratiba
endelevu kila siku.
“Inaweza kuwa ni muda wa chakula ama chai na muda mwingi ni kwa
ajili ya mazoezi hilo ndilo ambalo tunafanya kila siku,” anamaliza Shaban.
No comments:
Post a Comment