FEI TOTO ANA BALAA ZITO UWANJANI - Dizo Click

Dizo Click

Hot

Post Top Ad

Thursday 7 March 2024

FEI TOTO ANA BALAA ZITO UWANJANI

 


KIUNGO wa matajiri wa Dar, Azam FC Feisal Salum amekuwa kwenye ubora wake katika mechi za hivi karibuni ndani ya Ligi Kuu Bara akifanya kazi kubwa kwenye kutimiza majukumu yake.

Yote haya yanatokana na ushindani uliopo uwanjani huku Fei Toto akikamilisha kazi yake kwa umakini na kuwapa furaha mashabiki wa Azam FC wanaoifuatilia timu hiyo inayotumia Uwanja wa Azam Complex kwenye mechi za ushindani.

Nyota huyo anayevaa jezi namba 6 mgongoni ni chaguo la kwanza la Kocha Mkuu, Yusuph Dabo raia wa Senegel ambaye ameweka wazi kuwa kila mchezaji ndani ya kikosi hicho ana nafasi ya kufanya vizuri na makosa ambayo yamekuwa yanatokeo uwanjani wanayafanyia kazi eneo la mazoezi.

Azam FC imekuwa na mwendo mzuri kwenye mzunguko wa pili kwa kupata pointi kwenye mechi zote walizocheza Uwanja wa Azam Complex na safu ya ushambuliaji ikifunga mabao matano kwenye mechi mbili walizocheza wakiwa nyumbani.

Dabo amesema: “Kazi kubwa inafanyika kwa kila mchezaji kutimiza majukumu yake na ipo hivyo kila wakati jambo ambalo linaongeza nguvu kwenye kutimiza majukumu yetu na kupata ushindi ndani ya uwanja.

“Wakati mwingine tumekuwa tukishinwa kupata matokeo jambo ambalo linatokea hivyo kikubwa ni kuona tunakuwa kwenye mwendelezo mzuri kwa kuwa kinachohitajika ni ushindi na tunatambua kwamba ushindani ni mkubwa.

“Sio Feisal pekee bali kila mchezaji anatimiza majukumu yake hili ni jambo la msingi, pale ambapo tunashindwa kupata matokeo makosa tunafanyia kazi eneo la mazoezi ili kuwa bora kwa mechi zinazofuata,”.

Fei Toto kwenye mechi mbili zilizochezwa Uwanja wa Azam Complex alifunga jumla ya mabao matatu. Ubora wa Fei Toto ulichangia kupatikana kwa pointi nne kati ya pointi sita ambazo zilikuwa zinasakwa uwanjani ndani ya dakika 90.

Nyota huyo alifunga mabao mawili kwenye mchezo dhidi ya Dodoma Jiji uliochezwa Uwanja wa Azam Complex ambao baada ya dakika 90 ubao ulisoma Azam FC 4-1 Azam FC walipokomba pointi tatu jumlajumla.

Mchezo wa pili kufunga bao ilikuwa dhidi ya Coastal Union uliochezwa hapohapo Azam Complex ilikuwa ni Machi 6 ubao wa uliposoma Azam FC 1-1 Coastal Union wababe hao wakagawana pointi mojamoja.

Kwenye mchezo dhidi ya Coastal Union alifunga bao lililowapa pointi moja dakika za jioni kwa kuwa Azam FC walikuwa nyuma kwenye mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa dhidi ya Wagosi wa Kaya kutoka Tanga.

Fei alifunga bao hilo dakika ya 81 akiweka usawa bao ambalo lilifungwa na Semfuko Charlse dakika ya 68. Jumla anafikisha mabao 12 kwenye ligi akiwa ni kinara wa utupiaji mabao.

Mechi 20 Azam imecheza kwenye ligi ikiwa nafasi ya kwanza kibindoni imekusanya pointi 44 na safu ya ushambuliaji imetupia jumla ya mabao 45 msimu wa 2023/24.

Ikumbukwe kwamba licha ya kuwa ni kinara wa mabao akiwa nayo 12 kwenye ligi Fei ni mfungaji wa bao la kwanza ndani ya Azam FC kwenye ligi ilikuwa dhidi ya Tabora United mchezo uliochezwa Uwanja wa Azam Complex.

Katika mchezo huo bao la Fei Toto la ufunguzi lilifungwa dakika ya 3 ikiwa ni mwanzo wa msimu wa 2023/24 na rekodi nyingine aliyonayo ni mfungaji wa kwanza hat trick ndani ya Ligi Kuu Bara msimu wa 2023/24 alipofunga kwenye mchezo dhidi ya Tabora United.

Kazi kubwa ni kwenye mwendelezo wa kusaka pointi tatu ndani ya ligi huku kiungo huyo akiweka wazi kwamba kila mchezo kwao wanauchukulia kwa umuhimu ili kupata ushindi.

“Kila mchezo tunashirikiana na wachezaji wote ili kupata pointi tatu muhimu pale ambapo tunakosa huwa tunarejea kwenye uwanja wa mazoezi kufanyia kazi makosa yetu hiyo huwa inakuwa kazi ya benchi la ufundi kwenye kufanya maboresho yetu.

“Ushindani ni mkubwa na bado tunaendelea kushindana ili kupata matokeo, mashabiki wazidi kuwa pamoja nasi kwa kuwa kila wakati wapo nasi bega kwa bega katika hilo tunawaomba waendelee kuwa nasi,”

 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad