MWENDO ambao tulianza nao kwa wachezaji wa Timu ya Taifa Stars katika kuwania kufuzu Kombe la Mataifa Afrika, (CHAN) dhidi ya Uganda huohuo tumemaliza nao somo kubwa kwetu.
Kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Mkapa tuliona
kwamba tulipoteza kwa kufungwa bao 1-0 na uweza kujipa matumaini kwamba
tunakwenda kupata matokeo ugenini.
Ilikuwa ni maumivu kwa mara nyingine tena baada ya mchezo wa
pili pia kuisha kama ule wa awali kwa kupoteza mchezo tena.
Mabao 3-0 ambayo tumefungwa yamezima matumini ya Stars kuweza
kusonga mbele na sasa wamerejea kuweza kuanza mpago kazi upya kwa wakati ujao.
Tuliongea hapa kwamba sio kazi nyepesi kuweza kuwakabili Uganda
ambao nao walikuwa wanahitaji nafasi ya kuweza kusonga mbele.
Haijawezekana tumekwama na kutolewa kwa jumla ya mabao 4-0 hili
ni la maumivu kwa kila Mtanzania na muhimu kwa wachezaji kujiuliza kwa wakati
mwingine pale watakapoitwa kufanya kweli.
Mechi mbili bila kupata bao hii inatoa taswira kwamba taifa
linasumbuliwa na tatizo la ushambuliaji na kufungwa mabao pia inamaanisha bado
kwenye safu ya ulinzi kuna tatizo.
Hapo ndipo ambapo kazi inabidi ianze kufanyika kwa vitendo
kuanza kutengeneza vipaji vipya na kuvikuza vile ambavyo vipo kwa ajili ya
kuwatumia kwa wakati ujao.
Watanzania furaha yao ipo kwenye ushindi basi ni
muda wa kuwekeza kwa vitendo kwenye kuibua, kukuza, kuvilinda na
kuvitumia vipaji ambavyo vitaibuliwa sio kwa ajili ya leo bali kesho.
Ikiwa maandalizi yataanza kwa wakati huu kuendeleza vile ambavyo
tunavyo itatupa matokeo mazuri kesho kwa kuwa mpango kazi wetu utafanya kazi
nzuri na matokeo yataonekana.
Wachezaji wamekuwa wakijituma kutafuta matokeo ila wakati
mwingine wanashindwa kuyapata kutokana na kukutana na wapinzani ambao ni imara
zaidi yao.
Makosa ya mara kwa mara kwenye safu ya ulinzi na ushambuliaji
yanawapa nafasi wapinzani kujua namna ya kuwakabili Stars kwenye mechi ambazo
wanacheza nao.
Kwa sasa sio muda wa kuendelea kulaumu bali kuja na mpango kazi
ambao utatupa matokeo chanya baada ya miaka mitatu ijayo ama mitano.
Kuandaa timu bora hakuwezi kuleta majibu kwa muda mfupi wa
mwezi mmoja ama miwili lazima kuwe na mpango kazi wa miaka mitatu mpaka mitano
ambayo itawafanya wachezaji hao wawe ni kizazi kimoja.
Vipaji Tanzania vipo, uwezo wa wachezaji kupata matokeo kwenye
mechi zao nyumbani na ugenini upo lakini lazima wapewe maandalizi mazuri na
mbinu ambazo zitawafanya wafanye kazi kwa kujituma muda wote.
Kwa wachezaji ambao wataitwa kwenye mashindano mengine ndani ya
timu ya Taifa ya Tanzania jukumu lao liwe moja kujitoa bila kuogopa na
kutengeneza nafasi zaidi kushinda.
Ni mara chache kwa nafasi kupatikana hasa uwanjani na
ikipatikana kujirudia pia inakuwa ni ngumu hivyo ni muhimu kuweza kutumia
nafasi kwa umakini na kupata matokeo mapema.
Kwa mechi za nyumbani itakuwa somo kwa namna ambavyo Uganda wao
walikuwa wakifanya, muda wote wanacheza na kuleta presha kwa wapinzani.
Kwa hilo tuna amini wakati ujao kutakuwa na mabadiliko kwa
wachezaji katika kutumia uwanja wa nyumbani na ule wa ugenini.
Kazi bado ipo na ni muhimu kuwa na mpango kazi imara utakaotupa
matokeo na kuwapa furaha mashabiki na Watanzania kiujumla.

No comments:
Post a Comment