OFISA Habari wa Azam FC, Zakaria Thabit,'Zakazakazi' amesema kuwa wanaimani kubwa ya kufanya vizuri kwa msimu wa 2021/22 ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Timu hiyo inanolewa na Kocha Mkuu, George Lwandamina haanza kwenye mwendo mzuri msimu huu kama ambavyo ilifanya hivyo msimu uliopita wa 2020/22 ambapo baada ya mechi tano ilikuwa nafasi ya kwanza.
Kwa sasa Azam FC ipo nafasi ya nane ikiwa na pointi 7 na vinara ni Yanga wenye pointi 15 kibindoni.
Mchezo wao ujao kwenye ligi ni dhidi ya KMC unaotarajiwa kuchezwa Novemba 21, Uwanja wa Uhuru.
Ofisa huyo wa Habari ambaye yupo bega kwa bega na waandishi na ni mzee wa takwimu kichwani amesema kuwa wapo tayari kwa kupambana.
"Tupo tayari kwa ajili ya kuwa kwenye mapambano na hilo lipo wazi kutokana na wachezaji ambao wapo pamoja na benchi la ufundi.
"Kila mchezaji anajua kwamba kazi yake namba moja ni kupambana na kupata ushindi matokeo haya ya mwanzo ni mwanzo hayatakuwa hivi muda wote makosa tunayafanyia kazi,".
Moja ya maingizo mapya ndani ya timu hiyo ni pamoja na Rodgers Kola ambaye kibindoni ana bao moja alifunga mbele ya Namungo FC, Uwanja wa Azam Complex.

No comments:
Post a Comment