HESABU za Waafrika kuiona timu yao ya Morocco ikicheza fainali dhidi ya Timu ya Taifa ya Argentina zimekwama baada ya timu hiyo kupoteza mbele ya mabingwa watetezi wa kombe hilo Ufaransa.
Ubao wa Uwanja wa Al Bayt uliokusanya mashabiki 68,294 baada ya dakika 90 ulisoma Ufaransa 2-0 Morocco hivyo safari ya kuwaona wawakilishi kutoka Afrika Morocco wakicheza hatua ya fainali labda mpaka miaka minne ijayo.
Ni mabao ya Theo Hernandez dakika ya 5 likiwa ni bao la mapema lililowavuruga Morocco na bao la Randal Kolo Muani dakika ya 79 hili lilikuwa ni la pili na la kwanza kwa mchezaji huyo kufunga kwa timu yake ya taifa kwenye mashindano.
Mchezo huo wa hatua ya nusu fainali ulikuwa na ushindani mkubwa ambapo timu zote zilikuwa zinaonyesha uwezo kwenye kusaka matokeo ndani ya uwanja.
Kutinga kwao fainali Ufaransa kunawapa fursa ya kwenda kumenyana na Timu ya Taifa ya Argentina kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Dunia Qatar 2022 unaotarajiwa kuchezwa Jumapili.
Ufaransa walikuwa wajanja kwenye mchezo huo wa nusu fainali baada ya kusoma mbinu za Morocco ambayo iliushangaza ulimwengu kwa kuwafungashia virago Ureno yenye Cristiano Ronaldo baada ya Morocco kupata ushindi wa bao 1-0.
Ikumbukwe kwamba Morocco ni timu ya kwanza kutoka Afrika kuandika rekodi matata ya kutinga hatua ya nusu fainali Kombe la Dunia ilikuwa inasubiriwa kuandika rekodi ya kucheza fainali ya Kombe la Dunia jambo ambalo limegota mwisho.
Ufaransa ikiwa na Klyian Mbappe itamenyana na Argentina ya Lionel Messi ambayo ilishinda kwa mabao 3-0 dhidi ya Croatia kwenye mchezo wa hatua ya nusu fainali.
Mastaa hawa wawili Mbappe na Messi wote ni wachezaji wanaocheza timu moja ya Paris Saint-Germain hivyo vita yao itakuwa kwenye upande wa kusaka taji wakiwa na timu zao za taifa.
Ni vita ya Timu ya Taifa ya Argentina dhidi ya Ufaransa kwenye mchezo wa fainali ya Kome la Dunia na ni lazima mshindi mmoja apatikane kati ya nyota Lionel Messi atakayepambana na Kylian Mbappe ambaye ananukia kutwaa kiatu cha ufungaji bora akiwa ametupia mabao matano.
Messi mwenye miaka 35 anatajwa kulihitaji kwa ukaribu zaidi taji la Kombe la Dunia kwa sababu baada ya mchezo wao dhidi ya Croatia walipopata ushindi alisema kuwa anadhani Kombe hili la dunia litakuwa ni la mwisho kwake.
Baada ya kukwama kutinga hatua ya fainali sasa Morocco itacheza mchezo dhidi ya Timu ya Taifa ya Croatia kusaka mshindi wa nafasi ya pili mchezo unaotarajiwa kuchezwa Jumamosi.

No comments:
Post a Comment