NABI NA GADIEL YAWAKUTA WAFUNGIWA - Dizo Click

Dizo Click

Hot

Post Top Ad

Friday, 2 December 2022

NABI NA GADIEL YAWAKUTA WAFUNGIWA


KAMATI ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania imemfungia Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi mechi tatu.

Taarifa ambayo imetolewa leo Desemba 2,2022 imeeleza kuwa kocha huyo amepewa adhabu hiyo kutokana na kumshambulia mwamuzi wa kati na wa pembeni kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Ihefu.

Kwenye mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Highland Estate, ubao ulisoma Ihefu 2-1 Yanga.

Ikumbukwe kwamba ulikuwa ni mchezo wa kwanza kwa Yanga kupoteza mchezo msimu wa 2022/23.

 Pia beki wa Simba Gadiel Michael naye amefungiwa mechi tatu na faini ya laki tano sawa na Nabi ambaye naye amepigwa faini ya laki tano pia.

Gadiel yeye alipata adhabu hiyo kwa kosa la kulazimisha kuingia uwanjani saa 4:25 asubuhi kwa kilichoelezwa kuwa anakwenda kukagua uwanja.

Licha ya walinzi kumzuia Gadiel akiwa na watu wenye fulana fulana zenye nembo ya Simba kwa kuwa haukuwa muda husika, Gadiel alitumia hila na kuingia uwanjani ambapo taarifa imeeleza kuwa hakuonekana kwenda kukagua uwanja bali alienda eneo la katikati ya uwanja na kumwaga vitu vyenye asili ya unga.

Mchezo huo ulichezwa Uwanja wa Sokoine Novemba 23,2022 na ubao ulisoma Mbeya City 1-1 Simba.

Pia Simba imetozwa faini ya milioni moja kwa kosa la baadhi ya wachezaji wa timu kupitia mlango usio rasmi kuelekea mchezo wao dhidi ya Mbeya City.

Adhabu nyingine ambayo imetolewa ni kwa nyota wa Coastal Union, Maabad kwa kosa la kumshambulia mwamuzi wa kati na ametozwa faini ya laki tano kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Azam Complex, Azam FC 3-2 Coastal Union.

Nyota mwingine ambaye aliwahi kufungiwa mechi tatu na faini ya laki tano kutokana na masuala ya ushirikina ni Shafiq Batambuze wa Singida Big Stars ambaye alifanya hivyo kwenye mchezo dhidi ya Simba kwenye sare ya kufungana bao 1-1.


Taarifa ya kamati ilieleza kuwa nyota huyo aliingia uwanjani dakika 10 kabla ya mchezo na alionekana kumwaga vitu uwanjani.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad